Hamisi Babusa ni nani?

Dkt. Hamisi Omar Babusa ni Mhadhiri Wa Kiswahili, Taaluma Ya Lugha, Teknolojia Ya Elimu Na Masomo Ya Uanahabari, Mwandishi Wa Kazi za Kubuni na za Kitaaluma.

Alizaliwa Katika Kaunti ya Tana River, Sehemu za Pwani ya Kenya.

Alisomea Shule ya Msingi ya Garsen and Shule ya Upili ya Voi.

Baada ya Kufuzu Mtihani wa KCSE, alijiunga na Chuo kikuu cha Kenyatta kufanya Shahada ya Ualimu akiegemea sana Upande wa Kiswahili.

Alipokuwa mwanafunzi wa Chuo cha Kenyatta, Ndipo alipoendeleza na kujenga vipawa Vyake vya Kuandika, Kuigiza, Kunengua na Kuimba.

Alishiriki katika Sherehe za Kitamaduni za Chuo Cha kenyatta kwa miaka mingi hata upande wa Karate.

Alichapisha Kitabu chake cha Kwanza (Mazingira) mwaka 1995, akiwa bado mwanafunzi wa Chuo cha Kenyatta.(Tazama Sehemu ya machapisho kwa Maelezo Zaidi)

Baadaye alijisajili na Shahada ya Uzamili ya Kiswahili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta na akahafili Baada ya Miaka Miwili.

Baada ya Kuhafili na shahada ya uzamili aliajiriwa kama Mhadhiri Msaidizi.

Baadaye akaanza Kusomea Shahada ya Uzamifu ya Taaluma ya Lugha Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Akashinda Udhamini wa Kufundisha na Kuandika tasnifu yake Katika Chuo Kikuu cha St. Lawrence, Canton, NY, Marekani.

Alipokuwa katika Chuo cha St. Lawrence, Marekani, alifundisha Kiswahili (Msingi, Daraja la Pili na Daraja la Tatu), Fasihi na Tamaduni na Ngoma Afrika Mashariki.

Baada ya Miaka Miwili akarudi Kenya na Kuhafili Kisha akapewa kazi ya Uhadhiri ambayo Anaishikilia hadi leo.

Hamisi Babusa pia ni mwandishi maarufu wa kazi za Kibunifu na pia za Kitaaluma.

Katika uwanda wa Ubunifu ameandika Riwaya/Novela, Hadithi Fupi, Mashairi na pia Tamthilia Inayokuja karibuni.

Katika uwanda wa Kitaaluma ameandika Kamusi anuwai, Vitabu Vya Isimu and Miongozo ya Kazi za Fasihi.

Ameshiriki Katika Kuandaa Makongamano na Warsha Mbalimbali za Taaluma ya Lugha.

Amewasilisha Makala Mengi ya Kiakademia, Katika Makongamano Mengi ya Taaluma ya Lugha Marekani, Canada, Tanzania na Kenya.

Hamisi Babusa amewahi kuigiza katika filamu inyoitwa wrong number na kipindi cha runinga ya NTV kinachoitwa Pendo.

Hamisi Babusa ni muundaji wa vipindi vya Kiswahili anuwai vya redio na Runinga (drama, vichekesho n.k).

Amewahi kushiriki katika Vipindi Anuwai vya Kiswahili vya redio na Runinga kama vile: Bahari ya Lugha (Citizen Radio), Nuru ya Lugha (Radio Maisha), Mandhari ya Wiki na Mwamba wa Lugha (KTN News)

Yeye ni Nahodha wa Kipindi cha Mawimbi ya Lugha Kinachohusu Lugha na Fasihi ya Kiswahili katika Runinga ya KUTV.

Amewahi Kutafsiri kazi nyingi kutoka Kiingereza hadi kiswahili na pia Kiswahili hadi Kiingereza.

Amesimamia Wanafunzi kadhaa wa Shahada za juu Hadi Wakahitimu na kwa sasa anaendelea kusimamia Wengine ambao Wanaendelea Vizuri.

Ameandaa Kozi Fupi na Kufundisha Watangazaji, Maripota na Wahariri wa Kiswahili Kutoka Mashirika Mbalimbali ya Habari kama vile KTN na Nation Media Group.

Amefundisha Wanafunzi wa kigeni Lugha ya kiswahili.

Amefundisha Kozi Fupi za Wahadhiri Kuhusu mbinu za Kufundisha.

Mbali na Kufundisha na Kuandika, Hamisi Babusa pia ndiye Mkuu wa Kitengo cha Kutathmini Ubora wa Shughuli za Kiakademia Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.